historia ya tamthiliya ya kiafrika hususan tamthiliya ya Kiswahili kuanzia miaka ya 1960 hadi 2011

Hyiman (1975) anafasili fonetiki kuwa ni taaluma ambayo hususani huchunguza sauti ambazo hutumiwa na binadamu wakati wanapowasiliana kwa kutumia lugha.Massamba na wenzake (2004) wanakubaliana kuwa fonetiki ni tawi ambalo hujishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu zote zinazohusiana na utoaji,utamkaji, usafirishaji na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla.Habwe na Karanje (2004) wanakubaliana kuwa fonetiki ni taaluma ya kisayansi inayochunguza sauti za lugha ya wanadamu. Fonetiki hutimiza jukumu hili kwa kuchunguza jinsi sauti za lugha za wanadamu zinavyotamkwa, kusafirishwa kati ya kiungo cha mnenaji na sikio la msikilizaji na jinsi zinavyofasiriwa katika ubongo wa msikilizaji na kufasiliwa.Besha M. R (2007) anaeleza kuwa fonetiki ni taaluma inayoshughulikia na kuchunguza jinsi sauti jinsi zilivyo, zinavyotolewa na zinavyomfikia msikilizaji. Taaluma ya fonetiki huchunguza sauti zote ambazo zinaweza kutumika katika lugha yoyote ile na kutoa sifa za sauti hizo bila kujali vinatumika kwa lugha gani na kwa njia gani.Kutokana na fasili hizo hapo juu kutoka kwa wataalamu mbalimbali tunaweza kusema kuwa fonetiki ni tawi la isimu linaloshughulikia uchunguzi na uchambuzi wa sauti za lugha za binadamu pamoja na utoaji, utamkaji, usafirishaji na ufasili wa sauti hizo.Kwa upande wa fonolojia wataalamu mbalimbali wameweza kufasili maana ya fonolojia kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo;-Masamba na wenzie (2004) wanaeleza kuwa fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali za kugha za binadamu.TUKI (1990)  fonolojia ni tawi la isimu ambalo hushughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani.Yule (1985) naye anaeleza kuwa fonolojia kimsingi ni maelezo ya mifumo na ruwaza za sauti za lugha.Fudge (1973:46) anaeleza kuwa fonolojia ni kiwango kimojawapo cha lugha Fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha. Vipashio vya kifonolojia ni fonimu na alofoni zake.Hartman (1972) naye anaeleza kuwa fonolojia ni mtalaa wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani na uamilifu wao ndani ya mfumo wa lugha husika.Kutokana na fasili za wataalamu hao hapo juu ni wazi kuwa fonolojia ni utanzu wa isimu unaochunguza jinsi sauti za lugha zinavyofanya kazi katika lugha mbalimbali. Fonolojia hushughulikia jinsi sauti zinavyotumika, zinavyounganishwa na zinavyopangwa katika lugha yoyote mahususi ili kuunda tungo zenye maana.Pia kuna wataalamu mbalimbali walio jadili maana ya lugha,Trudgil (1974) anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.Weber (1985) anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa mawasiliano ya binadamu ambao hutumia mpangilio maalumu wa sauti kuunda vipashio vikubwa zaidi, kwa mfano mofimu, maneno na sentensi.Kwa ujumla lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zenye kubeba maana zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani kwa ajili ya mawasiliano.Japokuwa fonolojia na na fonetiki ni miongoni mwa matawi ya isimu lakini matawi haya yana tofautiana. Tofauti zake ni kama zifuatazo;Kwa upande wa fonetiki sauti za kifonetiki zinaponukuliwa huwakilishwa na mabano mraba [   ] wakati kwa upande wa fonolojia sauti za kifonolojia zinaponukuliwa huwakilishwa kwa alama za mshazari au mikwaju /   /.Katika fonetiki kipashio cha msingi cha fonetiki ni foni wakati katika fonolojia kipashio cha msingi ni fonimu.Wakati fonolojia inaachunguza sauti za lugha maalum na inayofahamika kama vile Kiswahili, Kiingereza, Kisafwa na lugha zingine kwa kuchunguza maneno na jinsi maneno hayo yanavyounganishwa na kutoa maana lakini kwa upande wa fonetiki yenyewe hushughulika na lugha zote na si lugha maalum kama ilivyo fonolojia. Fonetiki pia huchunguza uzalishaji wa  sauti za lugha kutoka katika bohari kuu la sauti.  Vilevile kwa upande wa fonetiki yenyewe hutumia nadharia za sayansi halisi kama vile fizikia, uhandisi, biolojia na hufaidi matokeo ya kiutafiti ya taaluma hizi. Kwa mfano ili kuelewa jinsi ala za sauti zinavyofanya kazi mwanafonetiki atafaidika na maelezo ya kibaiolojia kwani huhusu jinsi mwili wa mwanadamu unavyofanya kazi wakati kwa upande wa fonolojia yenyewe haitumii nadharia za sayansi kama ilivyo fonetiki bali huongozwa na taratibu na misingi ya nadharia ya Isimu.Fonetiki huchunguza sauti bila kuzingatia mfumo ambamo sauti hizo hutumika lakini kwa upande wa fonolojia yenyewe huchunguza sauti zilizo katika mfumo mmoja yaani lugha mahususi.  Hivyo basi fonetiki ni moja lakini fonolojia zipo nyingi kama lugha zenyewe zilivyo nyingi, kwa mfano hakuna fonetiki ya Kiswahili wala ya kiingereza bali kuna fonolojia ya Kiswahili na kiingereza. Kwa mfano sauti “x” ipo katika lugha ya kiingereza lakini katika lugha ya Kiswahili sauti hiyo haipo.Pia seti kuu ambayo ni fonetiki haina kikomo lakini fonolojia zote zina kikomo kwani inaaminika kuwa lugha nyingi duniani hutumia wastani wa sauti kati ya 20 na 40 tu. Kwa mfano Kiswahili kina fonimu 31 tu.Fonetiki huhakiki sauti za lugha bila kuzihusisha katika muktadha wa matumizi katika tungo. Hii ni kinyume na fonolojia ambayo huhakiki sauti za lugha kimatumizi. Kwa mfano kauli kuwa sauti [p] ni konsonanti ya kipasuo ya kanda tuli na ambayo ni ya midomo miwili ni kauli ya kifonetiki, hata hivyo tukisema kuwa sauti [p] hupatikana katika mfumo wa lugha ya Kiswahili na kuwa haiwezi kutokea mwishoni mwa neno la Kiswahili tunatoa kauli ya kifonolojia.Fonolojia huchunguza michakato mbalimbali na kanuni zinazohusiana na utokeaji wa sauti na miunganiko yake katika mifumo mahususi ya lugha kwa mfano mchakato wa udondoshaji neno /mupana/-[mpana] katika mfumo huu mchakato wa udondoshaji unatokea ambapo irabu u imedondoshwa kwa sababu imetanguliwa na konsonati ya mdomo ambayo ni nazali na kufuatiwa na konsonati halisi lakini kwa upande wa fonetiki yenyewe haiusiki na michakato ya utokeaji wa sauti kama mchakato wa udondoshaji wa hapo juu.Wakati fonolojia inahusika na vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na sauti, mpangilio  wake na uundaji wa maneno katika lugha mbalimbali na mfano wa vipengele hivyo ni kama vile matamshi, kiimbo, mkazo, lafudhi, silabi na wakaa na vilevile hata mfuatano wa mofimu katika kuunda maneno lakini katika fonetiki vingele hivyo havipo.Pamoja na kuwa na utofauti kati ya fonetiki na fonolojia kwa upande mwingine matawi haya ya isimu yana uhusiano mkubwa kama ifuatavyo;-Matawi haya yote mawili yaani fonetiki na fonolojia ni matawi ya isimu ambayo hushughulika  na uchunguzi na uchambuzi wa sauti za lugha katika viwango tofautitofauti wakati fonetiki huchunguza lugha kwa ujumla fonolojia yenyewe huchunguza lugha vilevile lakini ni lugha mahsusi au lugha fulani kwa maneno mengine kwa mfano lugha ya Kiswahili, lugha ya kingereza, kikongo na lugha nyingine zilizopo duniani.Fonetiki inaweza linganishwa na seti kuu ambayo hukusanya sauti nyingi sana duniani na kuziorodhesha na zingine lakini fonolojia ni sehemu tu ya seti kuu ambayo huchunguza sauti chache tu ya baadhi ya zile zilizoorodheshwa na wanafonetiki au kwa namna nyingine tunaweza kusema kuwa fonetiki ni msingi wa fonolojia kwa sababu sauti zinazoshughulikiwa na fonolojia ni baadhi tu ya zilizochotwa kutoka katika bohari kuu la sauti ambalo lipo katika fonetiki.Fonetiki na fonolojia ni matawi mawili ya isimu yaliyo jirani sana na wakati wote matawi haya hutegemeana na hukamilishana kwa mfano katika kufanya uchambuzi wa kifonetiki huusaidia sana fonolojia na katika kufanya uchambuzi wa kifonolojia husaidia sana fonetiki hivyo tunaweza kusema kwa namna nyingine kuwa yote haya matawi mawili fonetiki na fonolojia ni vipashio vya sauti na sauti hiyo ni sauti ya mwanadamu, na pia fonetiki na fonolojia zote ni faafu katika msepetuko wa lugha.Vilevile kwa upande wa lugha mbalimbali zilizopo duniani na zenyewe zina kufanana na kutofautiana kutokana na vipengele mbalimbali vinavyounda lugha hizo. Na kufanana kwake kunatokana na mambo yafuatayo;Lugha zote ni mfumo wa sauti za nasibu tu zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili ziweze kutumika katika mawasiliano miongoni mwa jamii hiyo husika. Hii ina maana kwamba sauti hizo zilitokea tu kwa bahati kwani hakuna kikao maalumu kilichokaa na kupanga kuwa neno hili litakuwa na maana hili au sauti hii itakuwa na maana hii. Kwa mfano neno mama ni la kiswahili, ujubha-kinyakyusa, ng’inesu-kiwanji, mai-kijita, na ayii! Kiiraq. Hayana uhusiano na wa moja kwa moja na kirejelewa mama kama mzazi wa kike katika lugha hizo hapo juu bali ni za nasibu tu.Lugha zote huchukua sauti chache kutoka katika bohari la sauti ambalo limebeba sauti nyingi na kila lugha huchukua sauti chache kulingana na mahitaji ya jamii yenyewe husika. Kwa mfano lugha ya Kiswahili imechukua sauti 31 wakati lugha ya Kiingereza ina sauti 44, kifaransa ina sauti 33. Lugha zote duniani hutolewa na viungo vya binadamu vijulikanavyo kama ala sauti. Ala hizo za sauti ni kama vile kaakaa gumu, kaakaa laini, ulimi, fizi mdomo na meno. Kwa mfano neno linalotamkwa kwa kutumia midomo ni “mama” na ndiyo maana mtu asiye na mdomo wa chini au mdomo wa juu hupata tabu wakati wa kutamka au wakati wa mazungumzo na hasa hupata tabu wakati wa kutamka vitamkwa mahususi vinavyo tamkwa kwa kutumia midomo.Lugha zote zilizopo duniani zinaambatana na utamaduni wa jamii fulani au jamii husika kulingana na matumizi au mahitaji ya jamii hiyo. Kwa mfano maneno kama upwa, mashua, ngalawa, kanzu na msuli yanaendana na utamaaduni wa watu wa pwani.Ufanano mwingine wa lugha mbalimbali zilizopo duniani ni kuwa lugha zote hujitosheleza kimatumizi kulingana na sauti ambazo imezichota kutoka katika bohari kuu la sauti.Ijapokuwa lugha nyingi zilizopo duniani hufanana kwa namna moja ama nyingine vilevile lugha hizo huweza kutofautiana pia na utofauti huo unajitokeza katika nyanja tofautitofauti kama inavyojidhihirisha kwenye maelezo yafuatayo;-Kila lugha asilia inachukua sauti chache tu kutoka katika bohari kuu la sauti hivyo sauti za lugha moja huweza kutofautiana na sauti za lugha nyingine kwa namna moja ama nyingine kwa mfano lugha ya kiswahili haijachukua sauti x, q na c kutoka katika bohari la sauti ilhali katika lugha ya kingereza sauti hizo zimechukuliwa na zinatambulika.Vilevile kila lugha ina kanuni zake ambazo ni kama kioo cha yale yaliyoko katika hazina ya kila lugha na mjua lugha, kwa mfano mjua Kiswahili yeyote anatambua kuwa [doa] na [toa] ni maneno mawili tofauti katika lugha hiyo na kila moja lina maana tofauti na hayawezi kubadirishwa, yaani mzungumzaji hawezi kuyachanganya katika semi za lugha hiyo, ni rahisi pia kueleza tofauti ya maneno hayo yanaletwa na nini ambayo ni kuwepo kwa sauti [d] badala ya [ t] lakini sauti nyingine zote zinafanana, zote ni vipasuo vya ufizi ila [d] ni ghuna na [t] ni si ghuna, tofauti inajitokeza ikiwa tunazungumzia lugha ya kipemba kwani wazungumzaji wa lugha hii wanaweka tofauti za msingi kati ya [t] na [th] ya kwanza ni kipasuo si ghuna cha ufizi  si pumuo na ya pili ni kipasuo si ghuna cha ufizi pumuo. Tofauti hizi ni za msingi kwa sababu maneno yafuatayo yana maana tofauti katika lugha 39 za kipemba [taa] na [thaa]neno la kwanza lina maana ya kifaa cha kutolea mwanga na la pili ni aina ya samaki. Na hii yote ni kutokana na kanuni na utaratibu wa lugha husika.Tofauti nyingine ni kuwa kila lugha ina mpangilio wake tofauti na lugha nyingine katika kuunda maneno au kwa maneno mengine tunaweza kusema sauti za msingi katika lugha fulani zinafumwa kwa njia tofauti katika kila lugha kwa mfano kila lugha zina kanunni maalum za jinsi sauti zinavyoweza kufuatana katika neno. Pia kuna minyumbusho tofauti ya kifonolojia inavyotokea katika matumizi ya sauti hizo kwa mfano katika Kiswahili mfuatano unaokubalika ni konsonanti + irabu (KI) au irabu + konsonanti + irabu (IKI) ni mwiko kwa konsonanti mbili kufuatana isipokuwa ikiwa ya mwanzo ni (m) au (n) na ikitokea  hivyo basi sauti hizo hupewa usilabi kama katika maneno mtu na nta.Utaratibu huu kwa baadhi ya wazungumzaji na katika Kiswahili cha maandishi hukiukwa kutokana na maneno ambayo yana asili ya lugha zisizo za kibantu kama askari, stakabadhi, skrubu, katika Kiswahili kisicho cha rasmi maneno haya hutamkwa asikari, sitakabadhi, sukurubu na hivyo kuhifadhi mfumo wa asili wa Kiswahili.Utofauti mwingine ni kuwa kila lugha ina sifa bainifu ya kwake. Sifa bainifu ya lugha moja siyo lazima iwe ile ile katika lugha nyingine. Kwa mfano kipemba na katika lugha ya Kithai ya Thailand [t] na [th] ni mofimu mbili tofauti kwa sababu sauti hizo zinatofautisha maneno katika lugha hizo kwa mfano [tam] ina maana ya ‘kutwanga’ na [tham] ina maana ya ‘kufanya’. Kwa maana hiyo basi mpumuo si sifa bainifu katika vipasuo vya lugha ya Kiswahili lakini ni sifa bainifu katika lugha za kipemba ya Zanzibar na Kithai ya Thailand. Katika lugha ya kiingereza mpumuo una hadhi tofauti katika maneno yafuatayo. Sauti [t] inatamkwa kwa maneno ya pekee katika kila neno. Kwa mfano [til] inatamkwa [thil], [still] inatamkwa [stil] hivyo katika neno la kwanza sauti ya kwanza ni kipasio si ghuna na ni cha ufizi pumuo na [th] ambapo katika neno la pili sauti ya pili ni kipasuo si ghuna cha ufizi lakini si pumuo. Lakini [t] tukichunguza mazingira, sauti hizi zinamotokea tunagundua kuwa [th] inatokea mwanzoni mwa neno ambapo [t] inafuata sauti.Konsonanti nyingine katika sauti hiyo ni [s] mazingira hayaingiliani lugha hii. Yaani sauti [t] haiwezi kutokea baada ya sauti [s] tofauti kubwa kati ya hadhi ya sauti hizo na zile za kipemba na kithai ni kwamba Kiingereza sauti [t] na [th] hazitumiki kutofautisha maneno katika lugha hiyo bali wazungumzaji wanajua ni wapi watumie moja na wapi watumie nyingine. Ikiwa mzungumzaji anatamka neno [till] kama [til] na neno [still] kama [sthill] wazungumzaji wazawa wa kiingereza watajua kuwa mzungumzaji ni mgeni wa lugha hiyo.Vile vile kuna utofauti wa namna ya uzungumaji wa maneno katika lugha mbalimbali zilizopo duniani. Hii ina maana kwamba kila lugha ina njia yake ya kuzalisha maneno. Kiswahili huzalisha maneno kwa njia ya kukopa maneno kutoka katika lugha yingine kwa mfano lugha ya Kiswahili imekopa maneno kama vile marhaba, shikamoo, shukran, alfajiri, magharibi na alasiri kutoka katika lugha ya Kiarabu. Pia lugha inajizalisha kwa njia ya kutohoa maneno kutoka lugha mbalimbali. Kwa mfano kinyakyusa kimetohoa maneno kama vile sukulu na isipuni kutoka katika lugha ya Kiingereza school na spoon.Vile vile tofauti nyingine ya lugha mbalimbali zilizopo duniani ni ile ya kuwa kila lugha ina mpangilio tofauti wa utokeaji wa sauti zake katika kuunda maneno mbalimbali yenye kubeba maana katika lugha husika. Kwa mfano silabi inaweza ikaanza na konsonanti ikafuata irabu lakini katika lugha nyingine mpangilio huo unakataa. Lugha nyingine zinakubali mpangilio wa konsonanti hata nne kufuatana lakini katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine za kibantu ni mara chache. Kwa mfano lugha ya kiingereza neno ‘embryo’ kuna sauti konsonanti nne zilizo fuatana yaani ‘mbry’ na vile vile kuna maneno yanayo weza kuundwa bila kuwepo na irabu. Kwa mfano ‘fly’, ‘sky’ ‘spy’ na ‘kry’.Tofauti nyingine ni kwamba kila lugha ina mfumo wake wa silabi. Hii ina maana kuwa mfumo wa silabi wa lugha moja hutofautiana na lugha nyingine. Kwa mfano mfumo wa silabi wa lugha za kibantu zilizo nyingi za silabi huru $KI$ lakini $  ni mpaka wa irabu lakini kwa baadhi ya lugha silabi zake ni funge mfano $KIK$ na kirefu cha KIK ni konsonanti irabu konsonanti wakati KI ni konsonanti irabu. Na hii ni sawa na kusema kwamba lugha nyingi za kibantu kwa kiasi kikubwa zina mfumo wa silabi huru.Katika lugha mbalimbali zilizopo duniani kila lugha ina mfumo wale wa irabu. Hii ina maana kwamba mfumo wa irabu wa lugha moja huweza kutofautiana na mfumo wa lugha nyingine kwa namna moja ama nyingine. Kwa mfano halisi ni kwamba kuna lugha zenye irabu saba, zingine zina irabu tano, zingine zina irabu tatu. Kutokana na ukweli kwamba kila lugha ina miliki na kutumia mfumo wake wa konsonanti hii inatokana na ukweli kwamba kila lugha ina kikomo chake cha matumizi ya sauti kutoka katika bohari kuu la sauti.Vile vil kila lugha ina utamaduni wake kulingana na mazingira husika hasa katika jamii inayotumia lugha hiyo. Kwa mfano lugha nyingi zinazo zungumzwa pwani huambatana na utamaduni wa ukanda huo. Kwa mfano maneno kama vile mashua, ngalawa, jahazi, upwa, kanzu, tasbihi na msuli huendana hasa na utamaduni wa wana jamii wa pwani ilhali watu wa bara hutofautiana na watu wa pwani kwa namna moja ama nyingine. Pia utamaduni wa wakulima na wafugaji lugha zao huendana na tamaduni zao maneno kama jembe, panga, maksai, matuta, swaga na mengineyo ya tamaduni za watu hawaNa mwisho kabisa kila lugha hujitosheliza kulingana na mahitaji ya jamii husika.Hivyo kwa maelezo toshelevu na dhahiri kama yalivyoelezwa hapo juu tunaweza kusema kwamba katika matawi mawili ya isimu yani fonetiki na fonolojia ni matawi ambayo yanafanya kazi kwa pamoja na kwa kutegemeana lakini ikiwa ni kwa kiasi kikubwa fonolojia hutegemea sana uwepo wa fonetiki ingawa kuna utofauti kwa namna fulani na kwa upande wa lugha zote mbalimbali zilizopo duniani kwa kiasi kikubwa lugha zote huunda mifumo tofauti tofauti na huweza kujitokeza kwa kiasi kikubwa kwa kutegemea uwepo wa jamii husika ya watumiaji wa lugha hiyo. Jamii ina nguvu kubwa na ushawishi kwa kiasi kikubwa katika kuunda msamiati mbalimbali ambayo itatumika na jamii hiyo na kutosheleza mahitaji ya walengwa. 
MAREJEO
Besha M, R. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu: Macmillan Aidan Ltd: Dar es salaam.
Habwe J na Karanja P (2004). Misingi ya Sarufi ya Kisswahili. Phoenix Publishers Ltd. Nairobi.
Massamba na wenzie (2004). Sarufi ya Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA) Sekondari na vyuo: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili chuo kikuu Dae es salaam.
Massamba D. P. B (1996). Phonological Theory, History and Development: Dar es salaam University Press.
Mgullu R. S (1999). Mtaala wa Isimu, Fonetiki Fonolojia na mofolojia ya Kiswahili: Longhorn publishers Ltd, Dar es salaam.

1 Response to "historia ya tamthiliya ya kiafrika hususan tamthiliya ya Kiswahili kuanzia miaka ya 1960 hadi 2011"

  1. Unknown says:
    26 March 2015 at 07:09

    SAFISAANA NDUGUZANGU....NIMEPATA UFAHAMU MKUBWA SANA JUU YA FONETIKI NA FONOLOJIA KWANI NIKO MWAKA WA KWANZA NACHUKUA LUGHA YA KISW NA ENGL...NASHUKURU KWA UPANA WAKE

Post a Comment