Hyiman (1975) anafasili fonetiki kuwa ni taaluma
ambayo hususani huchunguza sauti ambazo hutumiwa na binadamu wakati
wanapowasiliana kwa kutumia lugha.Massamba
na wenzake (2004) wanakubaliana kuwa fonetiki ni tawi ambalo hujishughulisha na
uchunguzi na uchambuzi wa taratibu zote zinazohusiana na utoaji,utamkaji,
usafirishaji na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla.Habwe
na Karanje (2004) wanakubaliana kuwa fonetiki ni taaluma ya kisayansi
inayochunguza sauti za lugha ya wanadamu. Fonetiki hutimiza jukumu hili kwa
kuchunguza jinsi sauti za lugha za wanadamu zinavyotamkwa, kusafirishwa kati ya
kiungo cha mnenaji na sikio la msikilizaji na jinsi zinavyofasiriwa katika
ubongo wa msikilizaji na kufasiliwa.Besha
M. R (2007) anaeleza kuwa fonetiki ni taaluma inayoshughulikia na kuchunguza
jinsi sauti jinsi zilivyo, zinavyotolewa na zinavyomfikia msikilizaji. Taaluma
ya fonetiki huchunguza sauti zote ambazo zinaweza kutumika katika lugha yoyote
ile na kutoa sifa za sauti hizo bila kujali vinatumika kwa lugha gani na kwa njia
gani.Kutokana
na fasili hizo hapo juu kutoka kwa wataalamu mbalimbali tunaweza kusema kuwa
fonetiki ni tawi la isimu linaloshughulikia uchunguzi na uchambuzi wa sauti za
lugha za binadamu pamoja na utoaji, utamkaji, usafirishaji na ufasili wa sauti
hizo.Kwa
upande wa fonolojia wataalamu mbalimbali wameweza kufasili maana ya fonolojia
kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo;-Masamba
na wenzie (2004) wanaeleza kuwa fonolojia ni tawi la isimu ambalo
hujishughulisha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo
hutumika katika mifumo mbalimbali za kugha za binadamu.TUKI
(1990) fonolojia ni tawi la isimu ambalo
hushughulikia uchambuzi wa mfumo wa sauti zinazotumiwa katika lugha fulani.Yule
(1985) naye anaeleza kuwa fonolojia kimsingi ni maelezo ya mifumo na ruwaza za
sauti za lugha.Fudge
(1973:46) anaeleza kuwa fonolojia ni kiwango kimojawapo cha lugha Fulani
kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha.
Vipashio vya kifonolojia ni fonimu na alofoni zake.Hartman
(1972) naye anaeleza kuwa fonolojia ni mtalaa wa sauti zinazotumiwa katika
lugha fulani na uamilifu wao ndani ya mfumo wa lugha husika.Kutokana
na fasili za wataalamu hao hapo juu ni wazi kuwa fonolojia ni utanzu wa isimu
unaochunguza jinsi sauti za lugha zinavyofanya kazi katika lugha mbalimbali.
Fonolojia hushughulikia jinsi sauti zinavyotumika, zinavyounganishwa na
zinavyopangwa katika lugha yoyote mahususi ili kuunda tungo zenye maana.Pia
kuna wataalamu mbalimbali walio jadili maana ya lugha,Trudgil
(1974) anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa
mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake.Weber
(1985) anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa mawasiliano ya binadamu ambao hutumia
mpangilio maalumu wa sauti kuunda vipashio vikubwa zaidi, kwa mfano mofimu,
maneno na sentensi.Kwa
ujumla lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zenye kubeba maana zilizokubaliwa na
jamii ya watu fulani kwa ajili ya mawasiliano.Japokuwa
fonolojia na na fonetiki ni miongoni mwa matawi ya isimu lakini matawi haya yana
tofautiana. Tofauti zake ni kama zifuatazo;Kwa
upande wa fonetiki sauti za kifonetiki zinaponukuliwa huwakilishwa na mabano
mraba [ ] wakati kwa upande wa fonolojia sauti za
kifonolojia zinaponukuliwa huwakilishwa kwa alama za mshazari au mikwaju / /.Katika
fonetiki kipashio cha msingi cha fonetiki ni foni wakati katika fonolojia
kipashio cha msingi ni fonimu.Wakati
fonolojia inaachunguza sauti za lugha maalum na inayofahamika kama vile
Kiswahili, Kiingereza, Kisafwa na lugha zingine kwa kuchunguza maneno na jinsi
maneno hayo yanavyounganishwa na kutoa maana lakini kwa upande wa fonetiki
yenyewe hushughulika na lugha zote na si lugha maalum kama ilivyo fonolojia. Fonetiki
pia huchunguza uzalishaji wa sauti za lugha
kutoka katika bohari kuu la sauti. Vilevile
kwa upande wa fonetiki yenyewe hutumia nadharia za sayansi halisi kama vile
fizikia, uhandisi, biolojia na hufaidi matokeo ya kiutafiti ya taaluma hizi.
Kwa mfano ili kuelewa jinsi ala za sauti zinavyofanya kazi mwanafonetiki
atafaidika na maelezo ya kibaiolojia kwani huhusu jinsi mwili wa mwanadamu
unavyofanya kazi wakati kwa upande wa fonolojia yenyewe haitumii nadharia za
sayansi kama ilivyo fonetiki bali huongozwa na taratibu na misingi ya nadharia
ya Isimu.Fonetiki
huchunguza sauti bila kuzingatia mfumo ambamo sauti hizo hutumika lakini kwa
upande wa fonolojia yenyewe huchunguza sauti zilizo katika mfumo mmoja yaani
lugha mahususi. Hivyo basi fonetiki ni
moja lakini fonolojia zipo nyingi kama lugha zenyewe zilivyo nyingi, kwa mfano
hakuna fonetiki ya Kiswahili wala ya kiingereza bali kuna fonolojia ya
Kiswahili na kiingereza. Kwa mfano sauti “x” ipo katika lugha ya kiingereza
lakini katika lugha ya Kiswahili sauti hiyo haipo.Pia
seti kuu ambayo ni fonetiki haina kikomo lakini fonolojia zote zina kikomo
kwani inaaminika kuwa lugha nyingi duniani hutumia wastani wa sauti kati ya 20
na 40 tu. Kwa mfano Kiswahili kina fonimu 31 tu.Fonetiki
huhakiki sauti za lugha bila kuzihusisha katika muktadha wa matumizi katika
tungo. Hii ni kinyume na fonolojia ambayo huhakiki sauti za lugha kimatumizi.
Kwa mfano kauli kuwa sauti [p] ni konsonanti ya kipasuo ya kanda tuli na ambayo
ni ya midomo miwili ni kauli ya kifonetiki, hata hivyo tukisema kuwa sauti [p]
hupatikana katika mfumo wa lugha ya Kiswahili na kuwa haiwezi kutokea mwishoni
mwa neno la Kiswahili tunatoa kauli ya kifonolojia.Fonolojia
huchunguza michakato mbalimbali na kanuni zinazohusiana na utokeaji wa sauti na
miunganiko yake katika mifumo mahususi ya lugha kwa mfano mchakato wa
udondoshaji neno /mupana/-[mpana] katika mfumo huu mchakato wa udondoshaji
unatokea ambapo irabu u imedondoshwa kwa sababu imetanguliwa na konsonati ya
mdomo ambayo ni nazali na kufuatiwa na konsonati halisi lakini kwa upande wa
fonetiki yenyewe haiusiki na michakato ya utokeaji wa sauti kama mchakato wa
udondoshaji wa hapo juu.Wakati
fonolojia inahusika na vipengele mbalimbali ambavyo vinahusiana na sauti,
mpangilio wake na uundaji wa maneno
katika lugha mbalimbali na mfano wa vipengele hivyo ni kama vile matamshi, kiimbo,
mkazo, lafudhi, silabi na wakaa na vilevile hata mfuatano wa mofimu katika
kuunda maneno lakini katika fonetiki vingele hivyo havipo.Pamoja
na kuwa na utofauti kati ya fonetiki na fonolojia kwa upande mwingine matawi
haya ya isimu yana uhusiano mkubwa kama ifuatavyo;-Matawi
haya yote mawili yaani fonetiki na fonolojia ni matawi ya isimu ambayo
hushughulika na uchunguzi na uchambuzi
wa sauti za lugha katika viwango tofautitofauti wakati fonetiki huchunguza
lugha kwa ujumla fonolojia yenyewe huchunguza lugha vilevile lakini ni lugha
mahsusi au lugha fulani kwa maneno mengine kwa mfano lugha ya Kiswahili, lugha
ya kingereza, kikongo na lugha nyingine zilizopo duniani.Fonetiki
inaweza linganishwa na seti kuu ambayo hukusanya sauti nyingi sana duniani na
kuziorodhesha na zingine lakini fonolojia ni sehemu tu ya seti kuu ambayo
huchunguza sauti chache tu ya baadhi ya zile zilizoorodheshwa na wanafonetiki
au kwa namna nyingine tunaweza kusema kuwa fonetiki ni msingi wa fonolojia kwa
sababu sauti zinazoshughulikiwa na fonolojia ni baadhi tu ya zilizochotwa
kutoka katika bohari kuu la sauti ambalo lipo katika fonetiki.Fonetiki
na fonolojia ni matawi mawili ya isimu yaliyo jirani sana na wakati wote matawi
haya hutegemeana na hukamilishana kwa mfano katika kufanya uchambuzi wa
kifonetiki huusaidia sana fonolojia na katika kufanya uchambuzi wa kifonolojia
husaidia sana fonetiki hivyo tunaweza kusema kwa namna nyingine kuwa yote haya
matawi mawili fonetiki na fonolojia ni vipashio vya sauti na sauti hiyo ni
sauti ya mwanadamu, na pia fonetiki na fonolojia zote ni faafu katika msepetuko
wa lugha.Vilevile
kwa upande wa lugha mbalimbali zilizopo duniani na zenyewe zina kufanana na
kutofautiana kutokana na vipengele mbalimbali vinavyounda lugha hizo. Na kufanana
kwake kunatokana na mambo yafuatayo;Lugha
zote ni mfumo wa sauti za nasibu tu zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili
ziweze kutumika katika mawasiliano miongoni mwa jamii hiyo husika. Hii ina
maana kwamba sauti hizo zilitokea tu kwa bahati kwani hakuna kikao maalumu
kilichokaa na kupanga kuwa neno hili litakuwa na maana hili au sauti hii
itakuwa na maana hii. Kwa mfano neno mama ni la kiswahili, ujubha-kinyakyusa,
ng’inesu-kiwanji, mai-kijita, na ayii! Kiiraq. Hayana uhusiano na wa moja kwa
moja na kirejelewa mama kama mzazi wa kike katika lugha hizo hapo juu bali ni
za nasibu tu.Lugha
zote huchukua sauti chache kutoka katika bohari la sauti ambalo limebeba sauti
nyingi na kila lugha huchukua sauti chache kulingana na mahitaji ya jamii
yenyewe husika. Kwa mfano lugha ya Kiswahili imechukua sauti 31 wakati lugha ya
Kiingereza ina sauti 44, kifaransa ina sauti 33. Lugha zote duniani hutolewa na viungo vya
binadamu vijulikanavyo kama ala sauti. Ala hizo za sauti ni kama vile kaakaa
gumu, kaakaa laini, ulimi, fizi mdomo na meno. Kwa mfano neno linalotamkwa kwa
kutumia midomo ni “mama” na ndiyo maana mtu asiye na mdomo wa chini au mdomo wa
juu hupata tabu wakati wa kutamka au wakati wa mazungumzo na hasa hupata tabu
wakati wa kutamka vitamkwa mahususi vinavyo tamkwa kwa kutumia midomo.Lugha
zote zilizopo duniani zinaambatana na utamaduni wa jamii fulani au jamii husika
kulingana na matumizi au mahitaji ya jamii hiyo. Kwa mfano maneno kama upwa,
mashua, ngalawa, kanzu na msuli yanaendana na utamaaduni wa watu wa pwani.Ufanano
mwingine wa lugha mbalimbali zilizopo duniani ni kuwa lugha zote hujitosheleza
kimatumizi kulingana na sauti ambazo imezichota kutoka katika bohari kuu la
sauti.Ijapokuwa
lugha nyingi zilizopo duniani hufanana kwa namna moja ama nyingine vilevile
lugha hizo huweza kutofautiana pia na utofauti huo unajitokeza katika nyanja
tofautitofauti kama inavyojidhihirisha kwenye maelezo yafuatayo;-Kila
lugha asilia inachukua sauti chache tu kutoka katika bohari kuu la sauti hivyo
sauti za lugha moja huweza kutofautiana na sauti za lugha nyingine kwa namna
moja ama nyingine kwa mfano lugha ya kiswahili haijachukua sauti x, q na c
kutoka katika bohari la sauti ilhali katika lugha ya kingereza sauti hizo
zimechukuliwa na zinatambulika.Vilevile
kila lugha ina kanuni zake ambazo ni kama kioo cha yale yaliyoko katika hazina
ya kila lugha na mjua lugha, kwa mfano mjua Kiswahili yeyote anatambua kuwa [doa]
na [toa] ni maneno mawili tofauti katika lugha hiyo na kila moja lina maana
tofauti na hayawezi kubadirishwa, yaani mzungumzaji hawezi kuyachanganya katika
semi za lugha hiyo, ni rahisi pia kueleza tofauti ya maneno hayo yanaletwa na
nini ambayo ni kuwepo kwa sauti [d] badala ya [ t] lakini sauti nyingine zote
zinafanana, zote ni vipasuo vya ufizi ila [d] ni ghuna na [t] ni si ghuna, tofauti
inajitokeza ikiwa tunazungumzia lugha ya kipemba kwani wazungumzaji wa lugha
hii wanaweka tofauti za msingi kati ya [t] na [th] ya kwanza ni
kipasuo si ghuna cha ufizi si pumuo na
ya pili ni kipasuo si ghuna cha ufizi pumuo. Tofauti hizi ni za msingi kwa
sababu maneno yafuatayo yana maana tofauti katika lugha 39 za kipemba [taa] na
[thaa]neno la kwanza lina maana ya kifaa cha kutolea mwanga na la
pili ni aina ya samaki. Na hii yote ni kutokana na kanuni na utaratibu wa lugha
husika.Tofauti
nyingine ni kuwa kila lugha ina mpangilio wake tofauti na lugha nyingine katika
kuunda maneno au kwa maneno mengine tunaweza kusema sauti za msingi katika
lugha fulani zinafumwa kwa njia tofauti katika kila lugha kwa mfano kila lugha
zina kanunni maalum za jinsi sauti zinavyoweza kufuatana katika neno. Pia kuna
minyumbusho tofauti ya kifonolojia inavyotokea katika matumizi ya sauti hizo
kwa mfano katika Kiswahili mfuatano unaokubalika ni konsonanti + irabu (KI) au
irabu + konsonanti + irabu (IKI) ni mwiko kwa konsonanti mbili kufuatana
isipokuwa ikiwa ya mwanzo ni (m) au (n) na ikitokea hivyo basi sauti hizo hupewa usilabi kama
katika maneno mtu na nta.Utaratibu
huu kwa baadhi ya wazungumzaji na katika Kiswahili cha maandishi hukiukwa
kutokana na maneno ambayo yana asili ya lugha zisizo za kibantu kama askari,
stakabadhi, skrubu, katika Kiswahili kisicho cha rasmi maneno haya hutamkwa
asikari, sitakabadhi, sukurubu na hivyo kuhifadhi mfumo wa asili wa Kiswahili.Utofauti
mwingine ni kuwa kila lugha ina sifa bainifu ya kwake. Sifa bainifu ya lugha
moja siyo lazima iwe ile ile katika lugha nyingine. Kwa mfano kipemba na katika
lugha ya Kithai ya Thailand [t] na [th] ni mofimu mbili tofauti kwa sababu
sauti hizo zinatofautisha maneno katika lugha hizo kwa mfano [tam] ina maana ya
‘kutwanga’ na [tham] ina maana ya ‘kufanya’. Kwa maana hiyo basi
mpumuo si sifa bainifu katika vipasuo vya lugha ya Kiswahili lakini ni sifa
bainifu katika lugha za kipemba ya Zanzibar na Kithai ya Thailand. Katika lugha ya kiingereza mpumuo una hadhi
tofauti katika maneno yafuatayo. Sauti [t] inatamkwa kwa maneno ya pekee katika
kila neno. Kwa mfano [til] inatamkwa [thil], [still] inatamkwa [stil] hivyo
katika neno la kwanza sauti ya kwanza ni kipasio si ghuna na ni cha ufizi pumuo
na [th] ambapo katika neno la pili sauti ya pili ni kipasuo si ghuna
cha ufizi lakini si pumuo. Lakini [t] tukichunguza mazingira, sauti hizi
zinamotokea tunagundua kuwa [th] inatokea mwanzoni mwa neno ambapo
[t] inafuata sauti.Konsonanti
nyingine katika sauti hiyo ni [s] mazingira hayaingiliani lugha hii. Yaani
sauti [t] haiwezi kutokea baada ya sauti [s] tofauti kubwa kati ya hadhi ya
sauti hizo na zile za kipemba na kithai ni kwamba Kiingereza sauti [t] na [th]
hazitumiki kutofautisha maneno katika lugha hiyo bali wazungumzaji wanajua ni
wapi watumie moja na wapi watumie nyingine. Ikiwa mzungumzaji anatamka neno
[till] kama [til] na neno [still] kama [sthill] wazungumzaji wazawa
wa kiingereza watajua kuwa mzungumzaji ni mgeni wa lugha hiyo.Vile
vile kuna utofauti wa namna ya uzungumaji wa maneno katika lugha mbalimbali
zilizopo duniani. Hii ina maana kwamba kila lugha ina njia yake ya kuzalisha
maneno. Kiswahili huzalisha maneno kwa njia ya kukopa maneno kutoka katika
lugha yingine kwa mfano lugha ya Kiswahili imekopa maneno kama vile marhaba, shikamoo,
shukran, alfajiri, magharibi na alasiri kutoka katika lugha ya Kiarabu. Pia
lugha inajizalisha kwa njia ya kutohoa maneno kutoka lugha mbalimbali. Kwa
mfano kinyakyusa kimetohoa maneno kama vile sukulu na isipuni kutoka katika
lugha ya Kiingereza school na spoon.Vile
vile tofauti nyingine ya lugha mbalimbali zilizopo duniani ni ile ya kuwa kila
lugha ina mpangilio tofauti wa utokeaji wa sauti zake katika kuunda maneno
mbalimbali yenye kubeba maana katika lugha husika. Kwa mfano silabi inaweza
ikaanza na konsonanti ikafuata irabu lakini katika lugha nyingine mpangilio huo
unakataa. Lugha nyingine zinakubali mpangilio wa konsonanti hata nne kufuatana
lakini katika lugha ya Kiswahili na lugha zingine za kibantu ni mara chache.
Kwa mfano lugha ya kiingereza neno ‘embryo’ kuna sauti konsonanti nne zilizo
fuatana yaani ‘mbry’ na vile vile kuna maneno yanayo weza kuundwa bila kuwepo
na irabu. Kwa mfano ‘fly’, ‘sky’ ‘spy’ na ‘kry’.Tofauti
nyingine ni kwamba kila lugha ina mfumo wake wa silabi. Hii ina maana kuwa
mfumo wa silabi wa lugha moja hutofautiana na lugha nyingine. Kwa mfano mfumo
wa silabi wa lugha za kibantu zilizo nyingi za silabi huru $KI$ lakini $ ni mpaka wa irabu lakini kwa baadhi ya lugha
silabi zake ni funge mfano $KIK$ na kirefu cha KIK ni konsonanti irabu
konsonanti wakati KI ni konsonanti irabu. Na hii ni sawa na kusema kwamba lugha
nyingi za kibantu kwa kiasi kikubwa zina mfumo wa silabi huru.Katika
lugha mbalimbali zilizopo duniani kila lugha ina mfumo wale wa irabu. Hii ina
maana kwamba mfumo wa irabu wa lugha moja huweza kutofautiana na mfumo wa lugha
nyingine kwa namna moja ama nyingine. Kwa mfano halisi ni kwamba kuna lugha
zenye irabu saba, zingine zina irabu tano, zingine zina irabu tatu. Kutokana na
ukweli kwamba kila lugha ina miliki na kutumia mfumo wake wa konsonanti hii
inatokana na ukweli kwamba kila lugha ina kikomo chake cha matumizi ya sauti kutoka
katika bohari kuu la sauti.Vile
vil kila lugha ina utamaduni wake kulingana na mazingira husika hasa katika
jamii inayotumia lugha hiyo. Kwa mfano lugha nyingi zinazo zungumzwa pwani
huambatana na utamaduni wa ukanda huo. Kwa mfano maneno kama vile mashua,
ngalawa, jahazi, upwa, kanzu, tasbihi na msuli huendana hasa na utamaduni wa
wana jamii wa pwani ilhali watu wa bara hutofautiana na watu wa pwani kwa namna
moja ama nyingine. Pia utamaduni wa wakulima na wafugaji lugha zao huendana na
tamaduni zao maneno kama jembe, panga, maksai, matuta, swaga na mengineyo ya
tamaduni za watu hawaNa
mwisho kabisa kila lugha hujitosheliza kulingana na mahitaji ya jamii husika.Hivyo
kwa maelezo toshelevu na dhahiri kama yalivyoelezwa hapo juu tunaweza kusema
kwamba katika matawi mawili ya isimu yani fonetiki na fonolojia ni matawi
ambayo yanafanya kazi kwa pamoja na kwa kutegemeana lakini ikiwa ni kwa kiasi
kikubwa fonolojia hutegemea sana uwepo wa fonetiki ingawa kuna utofauti kwa
namna fulani na kwa upande wa lugha zote mbalimbali zilizopo duniani kwa kiasi
kikubwa lugha zote huunda mifumo tofauti tofauti na huweza kujitokeza kwa kiasi
kikubwa kwa kutegemea uwepo wa jamii husika ya watumiaji wa lugha hiyo. Jamii
ina nguvu kubwa na ushawishi kwa kiasi kikubwa katika kuunda msamiati mbalimbali
ambayo itatumika na jamii hiyo na kutosheleza mahitaji ya walengwa.
MAREJEO
Besha
M, R. (2007). Utangulizi wa Lugha na
Isimu: Macmillan Aidan Ltd: Dar es salaam.
Habwe
J na Karanja P (2004). Misingi ya Sarufi
ya Kisswahili. Phoenix Publishers Ltd. Nairobi.
Massamba na wenzie (2004). Sarufi ya Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA)
Sekondari na vyuo: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili chuo kikuu Dae es salaam.
Massamba D. P. B (1996). Phonological Theory, History and Development:
Dar es salaam University Press.
Mgullu R. S (1999). Mtaala wa Isimu, Fonetiki Fonolojia na mofolojia ya Kiswahili: Longhorn
publishers Ltd, Dar es salaam.
www.gobookee.org/tofauti-baina
ya f...... saa 11:30 jioni tar 30/10/2013.
1 Comment